25 Ndipo wana wa Gadi na wana wa Reubeni wakanena na Musa, na kumwambia, Sisi watumishi wako tutafanya kama wewe bwana wangu utuagizavyo.
26 Watoto wetu, na wake wetu, na kondoo zetu, na ng’ombe zetu wote, watakuwa hapo katika miji ya Gileadi;
27 lakini sisi watumishi wako tutavuka, kila mume aliyevaa silaha za vita, mbele za BWANA, tuende vitani, kama wewe bwana wangu usemavyo.
28 Basi Musa akamwagiza Eleazari kuhani, na Yoshua mwana wa Nuni, na wakuu wa nyumba za mababa za kabila za wana wa Israeli, katika habari za watu hao.
29 Musa akawaambia, Kwamba wana wa Gadi, na wana wa Reubeni, watavuka Yordani pamoja nanyi, kila mtu aliyevaa silaha kwa vita, mbele za BWANA, nayo nchi itashindwa mbele yenu; ndipo mtawapa nchi ya Gileadi kuwa milki yao;
30 lakini ikiwa hawataki kuvuka pamoja nanyi, hali wamevaa silaha zao, ndipo watakuwa na milki zao kati yenu katika nchi ya Kanaani.
31 Wana wa Gadi, na wana wa Reubeni, wakajibu na kusema, Kama BWANA alivyotuambia sisi watumishi wako, ndivyo tutakavyofanya.