1 Kisha wale wakuu wa nyumba za mababa ya jamaa ya wana wa Gileadi, mwana wa Makiri, mwana wa Manase, katika jamaa za wana wa Yusufu, wakakaribia, na kunena mbele ya Musa, na mbele ya wakuu walio juu ya nyumba za mababa ya wana wa Israeli;
2 wakasema, BWANA alimwagiza bwana wangu awape wana wa Israeli nchi kwa kupiga kura iwe urithi wao; tena bwana wangu aliagizwa na BWANA awape binti za Selofehadi ndugu yetu huo urithi wa baba yao.
3 Wakiolewa na watu wa wana wa hizo kabila nyingine za wana wa Israeli, ndipo urithi wao utatwaliwa na kuondolewa katika urithi wa baba zetu, na hiyo kabila watakayotiwa ndani yake itaongezewa urithi wao; basi urithi huo utaondolewa katika kura ya urithi wetu.
4 Tena itakapokuwapo hiyo yubile ya wana wa Israeli, ndipo urithi wa hiyo kabila ambayo wamekuwa ndani yake utaongezewa huo urithi wao; hivyo urithi wao utaondolewa katika urithi wa kabila ya baba zetu.
5 Basi Musa akawaagiza wana wa Israeli kama neno la BWANA lilivyokuwa, akasema, Kabila ya wana wa Yusufu imenena yaliyo haki.