10 Tena siku ya nane ataleta hua wawili, au makinda mawili ya njiwa, aende nao kwa kuhani, hata mlangoni pa hema ya kukutania;
11 naye kuhani atasongeza mmoja kuwa sadaka ya dhambi, na wa pili kuwa sadaka ya kuteketezwa, naye atafanya upatanisho kwa ajili yake, kwa sababu aliingia kosani kwa ajili ya mfu, naye atatakasa kichwa chake siku iyo hiyo.
12 Kisha ataziweka kwa BWANA hizo siku za kujitenga kwake, naye ataleta mwana-kondoo mume wa mwaka wa kwanza, kuwa sadaka ya hatia; lakini hizo siku za kwanza hazitahesabiwa, kwa kuwa kule kujitenga kwake kulitiwa unajisi.
13 Na sheria ya Mnadhiri ni hii, zitakapotimia hizo siku za kujitenga kwake; ataletwa mlangoni pa hema ya kukutania;
14 naye atasongeza sadaka yake kwa BWANA, mwana-kondoo mmoja mume wa mwaka wa kwanza mkamilifu, kuwa sadaka ya kuteketezwa, na mwana-kondoo mmoja mke wa mwaka wa kwanza mkamilifu, kuwa sadaka ya dhambi, na kondoo mume mmoja mkamilifu kwa sadaka ya amani,
15 na kikapu cha mikate isiyotiwa chachu, mikate ya unga mwembamba iliyokandwa kwa mafuta, na mikate ya kaki isiyochachwa, iliyotiwa mafuta, pamoja na sadaka zake za unga, na sadaka zake za kinywaji.
16 Na kuhani atavisongeza mbele za BWANA, naye atasongeza sadaka yake ya dhambi, na sadaka yake ya kuteketezwa;