13 Na sheria ya Mnadhiri ni hii, zitakapotimia hizo siku za kujitenga kwake; ataletwa mlangoni pa hema ya kukutania;
14 naye atasongeza sadaka yake kwa BWANA, mwana-kondoo mmoja mume wa mwaka wa kwanza mkamilifu, kuwa sadaka ya kuteketezwa, na mwana-kondoo mmoja mke wa mwaka wa kwanza mkamilifu, kuwa sadaka ya dhambi, na kondoo mume mmoja mkamilifu kwa sadaka ya amani,
15 na kikapu cha mikate isiyotiwa chachu, mikate ya unga mwembamba iliyokandwa kwa mafuta, na mikate ya kaki isiyochachwa, iliyotiwa mafuta, pamoja na sadaka zake za unga, na sadaka zake za kinywaji.
16 Na kuhani atavisongeza mbele za BWANA, naye atasongeza sadaka yake ya dhambi, na sadaka yake ya kuteketezwa;
17 naye atamsongeza huyo kondoo mume kuwa dhabihu ya sadaka za amani kwa BWANA, pamoja na kikapu cha mikate isiyotiwa chachu; kisha kuhani atasongeza sadaka ya unga nayo, na sadaka yake ya kinywaji.
18 Naye Mnadhiri atakinyoa kichwa cha kujitenga kwake, mlangoni pa hema ya kukutania, kisha atatwaa hizo nywele za kichwa cha kujitenga kwake, na kuzitia katika moto ulio chini ya dhabihu ya sadaka za amani.
19 Kisha kuhani atautwaa mkono wa huyo kondoo mume uliotokoswa, na mkate mmoja usio chachu atautwaa kikapuni, na mkate mmoja wa kaki, naye ataitia mikononi mwa yule Mnadhiri, baada ya kunyoa kichwa cha kujitenga kwake;