11 Kisha BWANA akanena na Musa, na kumwambia, Watasongeza matoleo yao, kila mkuu kwa siku yake, kwa ajili ya kuiweka wakfu madhabahu.
12 Basi aliyetoa matoleo yake siku ya kwanza ni Nashoni mwana wa Aminadabu, wa kabila ya Yuda;
13 na matoleo yake yalikuwa sahani moja ya fedha, uzani wake ni shekeli mia na thelathini, na bakuli moja ya fedha uzani wake ni shekeli sabini, kwa shekeli ya mahali patakatifu; vyombo hivyo vyote viwili vilikuwa vimejaa unga mwembamba uliochanganywa na mafuta kuwa sadaka ya unga;
14 na kijiko kimoja cha dhahabu, uzani wake shekeli kumi, kimejaa uvumba;
15 ng’ombe mmoja mume mchanga, na kondoo mmoja mume, na mwana-kondoo mume mmoja wa mwaka wa kwanza, kuwa sadaka ya kuteketezwa;
16 mbuzi mume mmoja kuwa sadaka ya dhambi;
17 na kwa ajili ya dhabihu ya sadaka za amani, ng’ombe waume wawili, na kondoo waume watano, na mbuzi waume watano, na wana-kondoo watano waume wa mwaka wa kwanza; hayo ndiyo matoleo ya Nashoni mwana wa Aminadabu.