1 Lisikieni neno la BWANA, enyi wana wa Israeli; kwa maana BWANA ana mateto nao wakaao katika nchi, kwa sababu hapana kweli, wala fadhili, wala kumjua Mungu katika nchi.
2 Hapana neno ila kuapa kwa uongo, na kuvunja ahadi, na kuua, na kuiba, na kuzini; huruka mpaka, na damu hugusana na damu.
3 Kwa ajili ya hayo nchi itaomboleza, na kila mtu akaaye ndani yake atadhoofika, pamoja na wanyama wa kondeni na ndege wa angani; naam, samaki wa baharini pia wataondolewa.
4 Walakini asishindane mtu, wala mtu asikemee; maana watu wako ni kama wao washindanao na kuhani.
5 Na wewe utajikwaa wakati wa mchana, na nabii naye atajikwaa pamoja nawe wakati wa usiku; nami nitamwangamiza mama yako.