1 Kwa ajili hii mpende BWANA, Mungu wako, na kushika sikuzote mausia yake, na amri zake, na hukumu zake, na maagizo yake.
2 Nanyi leo jueni; kwa kuwa sisemi sasa na vijana vyenu, ambao hawakujua, wala hawakuona adhabu ya BWANA, Mungu wenu, ukuu wake, na mkono wake wa nguvu, na mkono wake ulionyoka,
3 na ishara zake, na kazi zake alizomfanya Farao mfalme wa Misri, na nchi yake yote, katikati ya Misri;
4 na alivyolifanya jeshi la Misri, farasi zao, na magari yao; na alivyowafunikiza maji ya Bahari ya Shamu walipokuwa wakiwaandamia, na alivyowaangamiza BWANA hata hivi leo;
5 na mambo aliyowafanyia ninyi barani, hata mkaja mahali hapa;
6 na alivyowafanya Dathani, na Abiramu, wana wa Eliabu mwana wa Reubeni; nchi ilivyofunua kinywa chake, ikawameza, na walio nyumbani mwao, na mahema yao, na kila kitu kilichokuwa hai kikiwafuata, katikati ya Israeli yote;