1 Aliyejeruhika konde, au aliyekatika tupu yake, asiingie mtu huyo katika mkutano wa BWANA.
2 Mwana wa haramu asiingie katika mkutano wa BWANA; hata kizazi cha kumi asiingie aliye wake katika mkutano wa BWANA.
3 Mwamoni wala Mmoabi wasiingie katika mkutano wa BWANA; wala hata kizazi cha kumi mtu wao asiingie katika mkutano wa BWANA milele;
4 kwa sababu hapo mlipotoka Misri hawakuwalaki na chakula wala maji njiani; na kwa kuwa walimwajiri juu yako Balaamu mwana wa Beori kutoka Pethori iliyo Mesopotamia, aje akuapize.
5 Lakini BWANA, Mungu wako, hakukubali kumsikiza huyo Balaamu; BWANA, Mungu wako, aliyageuza yale maapizo kuwa ni baraka, kwa vile alivyokupenda BWANA, Mungu wako.
6 Usitafute amani yao wala heri yao siku zako zote, milele.
7 Usimchukie Mwedomi; kwa kuwa ni ndugu yako; usimchukie Mmisri, kwa kuwa ulikuwa mgeni katika nchi yake.
8 Wana wao watakaozaliwa kizazi cha tatu na waingie katika mkutano wa BWANA.
9 Utakapotoka kwenda juu ya adui zako nawe u katika marago, jilinde na kila neno baya.
10 Akiwa kwenu mtu awaye yote asiyekuwa ni tohara kwa ajili ya yaliyomtukia usiku, na atoke nje ya kituo, wala asiingie ndani ya kituo;
11 lakini na iwe ikaribiapo jioni, yeye ataoga maji; na jua likiisha kuchwa ataingia ndani ya kituo.
12 Tena uwe na mahali nje ya kituo, kwa kutokea nje;
13 nawe uwe na jembe dogo katika silaha zako; napo uotamapo nje uchimbe kwa lile jembe, na kugeuka na kukifunika kikutokacho;
14 kwa kuwa BWANA. Mungu wako, yuatembea katika kituo akuokoe, na kukutolea adui zako mbele yako; kwa hiyo na kiwe kitakatifu kituo chako; asije akaona kitu kwako kisichokuwa safi, akageuka na kukuacha.
15 Usimrudishe kwa bwana wake mtumwa aliyejiponya kutoka kwa bwana wake kuja kwako;
16 na akae nawe, katikati yako, ndani ya malango yako mojawapo, mahali atakapochagua palipo pema machoni pake; usimwonee.
17 Pasiwe na kahaba katika binti za Israeli, wala pasiwe na hanithi katika wana wa Israeli wanaume.
18 Usilete ujira wa kahaba, wala mshahara wa mbwa, katika nyumba ya BWANA, Mungu wako, kwa ajili ya nadhiri yo yote; kwani haya ni machukizo kwa BWANA, Mungu wako, yote mawili.
19 Usimkopeshe ndugu yako kwa riba; riba ya fedha, riba ya vyakula, riba ya kitu cho chote kikopeshwacho kwa riba;
20 mgeni waweza kumkopesha kwa riba, ila usimkopeshe ndugu yako kwa riba; ili BWANA, Mungu wako, apate kukubarikia katika yote utiayo mkono wako, katika nchi uingiayo kuimiliki.
21 Utakapoweka nadhiri kwa BWANA, Mungu wako, usiwe mlegevu katika kuiondoa; kwa kuwa BWANA, Mungu wako, hataacha kuitaka kwako; nayo hivi itakuwa dhambi kwako.
22 Lakini ukijizuia usiweke nadhiri, haitakuwa dhambi kwako.
23 Yaliyotoka midomoni mwako yashike kuyafanya; kwa mfano wa ulivyomwekea nadhiri BWANA, Mungu wako, ni sadaka ya hiari uliyoahidi kwa kinywa chako.
24 Uingiapo katika shamba la mizabibu la jirani yako, utaweza kula zabibu za kukushibisha, kama upendavyo; ila usitie katika chombo chako.
25 Uingiapo katika mmea wa jirani yako waweza kuyapurura masuke kwa mkono wako; ila usisongeze mundu katika mmea wa jirani yako.