1 Hizi ndizo amri na hukumu mtakazotunza kuzifanya katika nchi aliyokupa BWANA, Mungu wa baba zako, uimiliki, siku zote mtakazoishi juu ya nchi.
2 Vunjeni kabisa mahali pote walipokuwa wakiitumikia miungu yao mataifa mtakayoyamiliki, juu ya milima mirefu, na juu ya vilima, na chini ya kila mti wenye majani mabichi;
3 nanyi zivunjeni madhabahu zao, zibomoeni nguzo zao, na maashera yao yateketezeni kwa moto, na sanamu za kuchonga za miungu yao zikateni; na jina lao lifutilieni mbali na mahali hapo.
4 Wala msimfanyie hivyo BWANA, Mungu wenu.
5 Lakini mahali atakapochagua BWANA, Mungu wenu, katika kabila zenu zote, apaweke jina lake, maana, ni makao yake, elekezeni nyuso zenu hapo, nawe wende huko;
6 pelekeni huko sadaka zenu za kuteketezwa, na dhabihu zenu, na zaka zenu, na sadaka ya kuinuliwa ya mikono yenu, na nadhiri zenu, na sadaka zenu za hiari, na wazaliwa wa kwanza wa makundi yenu ya ng’ombe na ya kondoo;
7 na huko mtakula mbele za BWANA, Mungu wenu, nanyi furahini katika yote mtakayotia mikono yenu, ninyi na wa nyumbani mwenu, aliyokubarikia BWANA, Mungu wako.
8 Msifanye kwa kufuata mambo yote tuyafanyayo hapa leo, kila mtu kama aonavyo vema machoni pake;
9 kwani hamjafikilia bado katika raha na urithi akupao BWANA, Mungu wako.
10 Lakini mtakapovuka Yordani na kukaa katika nchi anayowarithisha BWANA, Mungu wenu, akawapeni raha, akiwaokoa na adui zenu pande zote, mkakaa salama;
11 wakati huo itakuwa kwamba mahali pale atakapopachagua BWANA, Mungu wenu, alikalishe jina lake, hapo ndipo mtakapoleta kila kitu ninachowaamuru; sadaka zenu za kuteketezwa, na dhabihu zenu, na zaka zenu, na sadaka ya kuinuliwa ya mikono yenu, na nadhiri zenu zote teule mtakazoweka kwa BWANA.
12 Nanyi mtafurahi mbele za BWANA, Mungu wenu, ninyi, na wana wenu, na binti zenu, na watumishi wenu wanawaume na wanawake, na Mlawi aliyemo malangoni mwenu; kwa kuwa hana sehemu wala urithi kwenu.
13 Ujihadhari usitoe sadaka zako za kuteketezwa katika kila mahali upaonapo;
14 bali katika mahali atakapopachagua BWANA katika kabila zako mojawapo, ndipo utakapotoa sadaka zako za kuteketezwa, ndipo utakapotenda yote nikuamuruyo.
15 Pamoja na haya waweza kuchinja nyama na kula ndani ya malango yako yote, kwa kufuata yote yatamaniwayo na roho yako, kwa mfano wa baraka ya BWANA, Mungu wako, aliyokupa; aliye tohara na asiye tohara ana ruhusa kula katika nyama hiyo, kama ya paa na ya kulungu.
16 Lakini msiile damu; imwageni juu ya nchi kama maji.
17 Usile ndani ya malango yako zaka ya nafaka zako, wala ya divai yako, wala ya mafuta yako, wala wazaliwa wa kwanza wa makundi yako, ya ng’ombe wala ya kondoo, wala nadhiri zako uwekazo zo zote, wala sadaka zako za hiari, wala sadaka ya kuinuliwa ya mkono wako;
18 lakini hivyo mtakula mbele za BWANA, Mungu wako, mahali atakapochagua BWANA, Mungu wako, wewe, na mwanao mume na mke, na mtumwa wako mume na mke, na Mlawi aliye ndani ya malango yako; nawe furahi mbele za BWANA, Mungu wako, katika yote utakayotia mkono wako.
19 Jilinde nafsi yako usimwache Mlawi siku zote uishizo katika nchi yako.
20 BWANA, Mungu wako, atakapoongeza mpaka wako, kama alivyokuahidi, nawe utakaposema, Nataka kula nyama, kwa kuwa roho yako yatamani kula nyama; waweza kula nyama, kwa kufuata yote inayotamani roho yako.
21 Na mahali atakapochagua BWANA, Mungu wako, apaweke jina lake, pakiwa mbali nawe mno, ndipo utakapochinja katika kundi lako la ng’ombe na kondoo alilokupa BWANA kama nilivyokuagiza, nawe utakula ndani ya malango yako, kwa kufuata yote inayotamani roho yako.
22 Kama vile aliwavyo paa na kulungu, ndivyo utakavyoila nyama hii; asiyekuwa tohara na aliye tohara wataila pia.
23 Ila ujihadhari kwamba usile damu, kwani ile damu ndiyo uhai; na uhai usile pamoja na nyama.
24 Usiile; imwage juu ya nchi kama maji.
25 Usiile; ili upate kufanikiwa, na watoto wako baada yako utakapofanya yaliyoelekea machoni pa BWANA.
26 Ila vitu vyako vitakatifu ulivyo navyo, na nadhiri zako, uvitwae ukaende mahali atakapochagua BWANA;
27 nawe zisongeze sadaka zako za kuteketezwa, nyama na damu, juu ya madhabahu ya BWANA, Mungu wako; na damu ya dhabihu zako uimwage juu ya madhabahu ya BWANA, Mungu wako, na wewe utakula nyama yake.
28 Maneno haya nikuagizayo yote yatunze na kuyasikiza, ili upate kufanikiwa na watoto wako baada yako milele, hapo uyafanyapo yaliyo mema na kuelekea machoni pa BWANA, Mungu wako.
29 BWANA, Mungu wako, atakapoyakatilia mbali hayo mataifa mbele yako, huko uingiako kuyamiliki, nawe ukawatwaa, na kuketi katika nchi yao;
30 ujiangalie, usije ukanaswa ukawafuata, wakiisha kuangamizwa mbele yako; wala usije ukauliza habari za miungu yao, ukisema, Mataifa haya waitumikiaje miungu yao? Nami nifanye vivyo.
31 Usimtende kama haya BWANA, Mungu wako; kwani kila yaliyo machukizo kwa BWANA, ayachukiayo yeye, wameifanyia miungu yao; kwa maana hata wana wao na binti zao huiteketezea hiyo miungu yao ndani ya moto.
32 Neno niwaagizalo lo lote liangalieni kulifanya; usiliongeze, wala usilipunguze.