1 Makuhani Walawi, kabila yote ya Lawi, wasiwe na fungu wala urithi pamoja na Israeli; watakula sadaka za BWANA zifanywazo kwa moto, na urithi wake.
2 Wala wasiwe na urithi kati ya ndugu zao; BWANA ndiye urithi wao, kama alivyowaambia.
3 Na hii itakuwa haki ya makuhani kwa watu hao wasongezao sadaka, ikiwa ni ng’ombe au kondoo wampe kuhani mkono, na mashavu mawili, na tumbo.
4 Malimbuko ya nafaka zako, na divai yako, na mafuta yako, na manyoya ya kwanza ya kondoo zako, umpe.
5 Kwani BWANA, Mungu wako, amemchagua katika kabila zako zote, asimame atumike kwa jina la BWANA, yeye na wanawe milele.
6 Na akija Mlawi atokaye katika malango yako mojawapo, katika Israeli yote alipokuwa akikaa, akaja kwa mapenzi yote ya nafsi yake mahali atakapochagua BWANA;
7 na atumike kwa jina la BWANA, Mungu wake, kama wafanyavyo ndugu zake wote, Walawi wasimamao huko mbele za BWANA.
8 Wawe na fungu sawasawa la kula, pamoja na haya yaliyomfikilia kwa kuuzwa urithi wa baba zake.
9 Utakapokwisha kuingia katika nchi akupayo BWANA, Mungu wako usijifunze kutenda kwa mfano wa machukizo ya mataifa yale.
10 Asionekane kwako mtu ampitishaye mwanawe au binti yake kati ya moto, wala asionekane mtu atazamaye bao, wala mtu atazamaye nyakati mbaya, wala mwenye kubashiri, wala msihiri,
11 wala mtu alogaye kwa kupiga mafundo, wala mtu apandishaye pepo, wala mchawi, wala mtu awaombaye wafu.
12 Kwa maana mtu atendaye hayo ni chukizo kwa BWANA; kisha ni kwa sababu ya hayo BWANA, Mungu wako, anawafukuza mbele yako.
13 Uwe mkamilifu kwa BWANA, Mungu wako.
14 Maana mataifa haya utakaowamiliki huwasikiliza wanaoshika nyakati mbaya na kutazama bao; bali wewe, BWANA, Mungu wako, hakukupa ruhusa kutenda hayo.
15 BWANA, Mungu wako, atakuondokeshea nabii miongoni mwa ndugu zako kama nilivyo mimi; msikilizeni yeye.
16 Kama vile ulivyotaka kwa BWANA, Mungu wako, huko Horebu, siku ya kusanyiko, ukisema, Nisisikie tena sauti ya BWANA, Mungu wangu, wala nisiuone tena moto huu mkubwa, nisije nikafa.
17 BWANA akaniambia, Wametenda vema kusema walivyosema.
18 Mimi nitawaondokeshea nabii miongoni mwa ndugu zao mfano wako wewe, nami nitatia maneno yangu kinywani mwake, naye atawaambia yote nitakayomwamuru.
19 Hata itakuwa, mtu asiyesikiliza maneno yangu atakayosema yule kwa jina langu, nitalitaka kwake.
20 Lakini nabii atakayenena neno kwa kujikinai kwa jina langu, ambalo sikumwagiza kulinena, au atakayenena katika jina la miungu mingine, nabii yule atakufa.
21 Nawe ukisema moyoni mwako, Tutajuaje neno asilolinena BWANA?
22 Atakaponena nabii kwa jina la BWANA, lisifuate jambo lile wala kutimia, hilo ndilo neno asilolinena BWANA; kwa kujikinai amelinena huyo nabii, usimwogope