1 Ninyi mmekuwa wana wa BWANA, Mungu wenu; msijitoje miili yenu, wala msifanye upaa katikati ya macho yenu kwa ajili ya aliyekufa.
2 Kwa kuwa u taifa takatifu kwa BWANA, Mungu wako, na BWANA amekuchagua kuwa watu wake hasa, kuliko mataifa yote yaliyo juu ya uso wa nchi.
3 Usile kitu cho chote kichukizacho.
4 Wanyama mtakaokula ni hawa ng’ombe, na kondoo, na mbuzi,
5 kulungu, na paa, na kongoni, na mbuzi wa mwitu, na paa mweupe, na pofu, na mbuzi wa mlima;
6 na kila mnyama aliyepasuliwa ukwato, ukapasuka ukwato wake zikawa mbili, naye ni mnyama mwenye kucheua akatafuna tena, katika wanyama wote, ndiye mnyama mtakayemla.