36 BWANA atakupeleka wewe, na mfalme wako utakayemweka juu yako, kwa taifa usilolijua wewe wala baba zako; nawe huko utatumikia miungu mingine ya miti na mawe.
37 Nawe utakuwa ushangao, na mithali, na dharau, kati ya mataifa yote huko atakakokuongoza BWANA.
38 Mbegu nyingi utazichukua nje shambani, lakini utavuna haba, kwa kuwa nzige watazila.
39 Utapanda mizabibu na kuitengeza, wala hutakunywa katika divai yake, wala kuichuma kwani italiwa na mabuu.
40 Utakuwa na mizeituni katika mipaka yako yote usijipake mafuta yake; kwa kuwa mzeituni wako utapukutika.
41 Utazaa wana na binti, lakini hawatakuwa wako wewe; kwa sababu watakwenda utumwani.
42 Miti yako yote, na mazao ya nchi yako, nzige watakuwa nayo.