3 Sikiza basi, Ee Israeli, ukaangalie kuzitenda; upate kufanikiwa, mpate kuongezeka sana, kama BWANA, Mungu wa baba zako, alivyokuahidi, katika nchi ijaayo maziwa na asali.
4 Sikiza, Ee Israeli; BWANA, Mungu wetu, BWANA ndiye mmoja.
5 Nawe mpende BWANA, Mungu wako, kwa moyo wako wote, na kwa roho yako yote, na kwa nguvu zako zote.
6 Na maneno haya ninayokuamuru leo, yatakuwa katika moyo wako;
7 nawe uwafundishe watoto wako kwa bidii, na kuyanena uketipo katika nyumba yako, na utembeapo njiani, na ulalapo, na uondokapo.
8 Yafunge yawe dalili juu ya mkono wako, nayo yatakuwa kama utepe katikati ya macho yako.
9 Tena yaandike juu ya miimo ya nyumba yako, na juu ya malango yako.