1 Amri hii ninayokuamuru leo mtaishika kuitenda, mpate kuishi na kuongezeka, na kuingia katika nchi ile ambayo BWANA aliwaapia baba zenu; nanyi mtaimiliki.
2 Nawe utaikumbuka njia ile yote BWANA, Mungu wako aliyokuongoza miaka hii arobaini katika jangwa, ili akutweze, kukujaribu kuyajua yaliyo moyoni mwako, kwamba utashika amri zake, au sivyo.
3 Akakutweza, akakuacha uone njaa, akakulisha kwa mana, usiyoijua wewe wala baba zako hawakuijua; apate kukujulisha ya kuwa mwanadamu haishi kwa mkate tu, bali huishi kwa kila litokalo katika kinywa cha BWANA.
4 Mavazi yako hayakuchakaa, wala mguu wako haukuvimba, miaka hiyo arobaini.
5 Nawe fikiri moyoni mwako, ya kuwa kama vile baba amrudivyo mwanawe, ndivyo BWANA, Mungu wako, akurudivyo.
6 Nawe uzishike amri za BWANA, Mungu wako, upate kwenda katika njia zake, na kumcha.
7 Kwa kuwa BWANA, Mungu wako, yuakuingiza katika nchi nzuri, nchi yenye vijito vya maji, na chemchemi, na visima, vibubujikavyo katika mabonde na milima;