9 Wamisri wakafuata nyuma yao, farasi zote na magari yote ya Farao, na askari zake wenye kupanda farasi, na jeshi lake, nao wakawapata hali wamepanga pale karibu na bahari, karibu na Pi-hahirothi, kukabili Baal-sefoni.
10 Hata Farao alipokaribia, wana wa Israeli wakainua macho yao, na tazama, Wamisri wanakuja nyuma yao; wakaogopa sana; wana wa Israeli wakamlilia BWANA.
11 Wakamwambia Musa, Je! Kwa sababu hapakuwa na makaburi katika Misri umetutoa huko ili tufe jangwani? Mbona umetutendea haya, kututoa katika nchi ya Misri?
12 Neno hili silo tulilokuambia huko Misri, tukisema, Tuache tuwatumikie Wamisri? Maana ni afadhali kuwatumikia Wamisri kuliko kufa jangwani.
13 Musa akawaambia watu, Msiogope, simameni tu, mkauone wokovu wa BWANA atakaowafanyia leo; kwa maana hao Wamisri mliowaona leo hamtawaona tena milele.
14 BWANA atawapigania ninyi, nanyi mtanyamaza kimya.
15 BWANA akamwambia Musa, Mbona unanililia mimi? Waambie wana wa Israeli waendelee mbele.