10 BWANA akamwambia Musa, Enenda kwa watu hawa, ukawatakase leo na kesho, wakazifue nguo zao,
11 wawe tayari kwa siku ya tatu; maana siku ya tatu BWANA atashuka katika mlima wa Sinai machoni pa watu hawa wote.
12 Nawe utawawekea mipaka watu hawa pande zote, ukisema, Jihadharini, msipande mlima huu, wala msiuguse, hata mapambizo yake; kila mtu atakayeugusa mlima huu, bila shaka atauawa.
13 Mkono wa mtu awaye yote usimguse mtu huyo, ila hakika yake atapigwa kwa mawe, au kupigwa kwa mkuki; kwamba ni mnyama au kwamba ni mwanadamu, hataishi. Hapo panda itakapotoa sauti kwa kufuliza ndipo watakapoukaribia mlima.
14 Musa akatelemka mlimani akawaendea watu akawatakasa, nao wakafua nguo zao.
15 Akawaambia watu; Mwe tayari siku ya tatu; msimkaribie mwanamke.
16 Ikawa siku ya tatu, wakati wa asubuhi, palikuwa na ngurumo na umeme, na wingu zito juu ya mlima, na sauti ya baragumu iliyolia sana. Watu wote waliokuwa kituoni wakatetemeka.