2 Nao walipokuwa wameondoka Refidimu na kufika jangwa la Sinai, wakatua katika lile jangwa; Israeli wakapiga kambi huko wakiukabili mlima.
3 Musa akapanda kwa Mungu, na BWANA akamwita toka mlima ule, akisema, Utawaambia nyumba ya Yakobo, na kuwaarifu wana wa Israeli, maneno haya;
4 Mmeona jinsi nilivyowatendea Wamisri, na jinsi nilivyowachukua ninyi juu ya mbawa za tai, nikawaleta ninyi kwangu mimi.
5 Sasa basi ikiwa mtaitii sauti yangu kweli kweli, na kulishika agano langu, hapo ndipo mtakapokuwa tunu kwangu kuliko makabila yote ya watu; maana dunia yote pia ni mali yangu,
6 nanyi mtakuwa kwangu ufalme wa makuhani, na taifa takatifu. Hayo ndiyo maneno utakayowaambia wana wa Israeli.
7 Musa akaenda akawaita wazee wa watu, akawafunulia maneno hayo yote, BWANA aliyokuwa amemwagiza.
8 Watu wote wakaitika pamoja wakisema, Hayo yote aliyoyasema BWANA tutayatenda. Naye Musa akamwambia BWANA maneno ya hao watu.