9 Usimwonee mgeni; maana, ninyi mwajua moyo wa mgeni ulivyo, kwa kuwa ninyi mlikuwa wageni katika nchi ya Misri.
10 Utapanda mbegu katika nchi yako muda wa miaka sita na kuyavuna maongeo yake;
11 lakini mwaka wa saba utaiacha nchi ipumzike na kutulia; hao maskini miongoni mwa watu wako wapate kula; na hicho watakachosaza wao, wapate kula wanyama wa kondeni. Utafanya vivyo katika shamba lako la mizabibu, na katika shamba lako la mizeituni.
12 Siku sita utafanya kazi yako, na siku ya saba utapumzika; ili kwamba ng’ombe wako na punda wako wapate kupumzika, kisha mwana wa mjakazi wako na mgeni wapate kuburudika.
13 Yaangalieni hayo yote niliyowaambia; wala msitaje kabisa majina ya miungu mingine, wala yasisikizwe kutoka kinywani mwako.
14 Mara tatu kila mwaka utaniwekea sikukuu.
15 Utaiweka sikukuu ya mikate isiyotiwa chachu; utakula mikate isiyochachwa muda wa siku saba kama nilivyokuagiza, kwa wakati uliowekwa, mwezi wa Abibu (kwa maana ndio mwezi uliotoka Misri); wala hapana mtu atakayeonekana mbele yangu na mikono mitupu;