1 Nawe uwafanyie jambo hili, ili kuwatakasa, wapate kunitumikia mimi katika kazi ya ukuhani; twaa ng’ombe mmoja mume kijana, na kondoo waume wawili walio wakamilifu,
2 na mkate usiotiwa chachu, na maandazi yasiyotiwa chachu yaliyokandwa kwa mafuta, na kaki zisizotiwa chachu zilizotiwa mafuta; utazifanya za unga mzuri mwembamba wa ngano.
3 Nawe vitie vyote katika kikapu, uvilete ndani ya kikapu, pamoja na huyo ng’ombe, na hao kondoo waume wawili.
4 Kisha mlete Haruni na wanawe hata mlangoni pa hema ya kukutania, ukawaoshe kwa maji.
5 Kisha twaa hayo mavazi na kumvika Haruni; itie kanzu, na joho ya naivera, na naivera, na kifuko cha kifuani, na kumkaza kwa huo mshipi wa naivera uliosukwa kwa ustadi;
6 nawe mvike kile kilemba kichwani, na ile taji takatifu utaitia katika kile kilemba.
7 Ndipo utakapotwaa hayo mafuta ya kutiwa, na kummiminia kichwani mwake, na kumtia mafuta.