21 Au kwamba huwapi ruhusa watu wangu, tazama, nitaleta wingi wa mainzi juu yako wewe, na juu ya watumishi wako, na juu ya watu wako, nao wataingia ndani ya nyumba zako; na nyumba za Wamisri zitajawa na wingi wa mainzi, na nchi nayo ambayo wa juu yake.
22 Nami siku hiyo nitatenga nchi ya Gosheni, watu wangu wanayokaa, ili hao mainzi wasiwe huko; ili kwamba upate kujua wewe ya kuwa mimi ndimi BWANA kati ya dunia.
23 Nami nitatia mpaka kati ya watu wangu na watu wako; ishara hiyo italetwa kesho.
24 BWANA akafanya; wakaja wingi wa mainzi kwa uzito sana, wakaingia nyumbani mwa Farao, na katika nyumba za watumishi wake, tena katika nchi yote ya Misri; nayo nchi iliharibiwa kwa ajili ya wale mainzi.
25 Farao akawaita Musa na Haruni akawaambia, Endeni mkamtolee Mungu wenu dhabihu ndani ya nchi hii.
26 Musa akasema, Haitupasi kufanya hivyo; kwa kuwa tutamchinjia sadaka BWANA, Mungu wetu, na hayo machukizo ya Wamisri; je! Tutachinja sadaka ya hayo machukizo ya Wamisri mbele ya macho yao, wasitupige kwa mawe?
27 La, tutakwenda safari ya siku tatu jangwani, tumchinjie dhabihu BWANA, Mungu wetu, kama atakavyotuagiza.