7 Waganga nao wakafanya mfano wa hayo kwa uganga wao; na kuwaleta vyura juu ya nchi ya Misri.
8 Ndipo Farao akawaita Musa na Haruni na kuwaambia, Mwombeni BWANA, ili awaondoe vyura hawa kwangu mimi na kwa watu wangu; nami nitawapa watu ruhusa waende zao, ili wamtolee BWANA dhabihu.
9 Musa akamwambia Farao, Haya, ujitukuze juu yangu katika jambo hili; sema ni lini unapotaka nikuombee wewe, na watumishi wako, na watu wako, ili hao vyura waangamizwe watoke kwako wewe na nyumba zako, wakae ndani ya mto tu.
10 Akamwambia, Kesho, Akasema, Na yawe kama neno lako; ili upate kujua ya kwamba hapana mwingine mfano wa BWANA, Mungu wetu.
11 Hao vyura wataondoka kutoka kwako wewe na nyumba zako, na watumishi wako, na watu wako; watasalia mtoni tu.
12 Basi Musa na Haruni wakatoka kwa Farao; Musa akamlilia BWANA katika jambo la hao vyura aliokuwa amewaleta juu ya Farao.
13 BWANA akafanya sawasawa na neno la Musa; na hao vyura wakafa kutoka katika zile nyumba, na katika viwanja, na katika mashamba.