4 Nikajifanyizia kazi zilizo kubwa; nikajijengea nyumba; nikajipandia mashamba ya mizabibu;
5 nikajifanyizia bustani na viunga, na kuipanda humo miti yenye matunda ya kila namna;
6 nikajifanyizia birika za maji, ya kuunyweshea mwitu mlimopandwa miti michanga.
7 Nami nikanunua watumwa na wajakazi, nikawa na wazalia nyumbani mwangu; tena nikawa na mali nyingi za ng’ombe na kondoo, kupita wote walionitangulia katika Yerusalemu;
8 tena nikajikusanyia fedha na dhahabu, na tunu za kifalme na za kutoka katika majimbo. Nikajipatia waimbaji, waume kwa wake, nao wale ambao wanadamu wanawatunuka, masuria wengi sana.
9 Basi nikawa mkuu, nikaongezeka kupita wote walionitangulia katika Yerusalemu; pia hekima yangu nikakaa nayo.
10 Wala sikuyanyima macho yangu cho chote yalichokitamani; wala sikuuzuia moyo wangu katika furaha yo yote; maana moyo wangu ulifurahi kwa sababu ya kazi yangu yote, na hii ilikuwa sehemu yangu katika kazi yangu yote.