1 Basi Dina, binti Lea, ambaye Lea alimzalia Yakobo, akatoka kuwaona binti za nchi.
2 Shekemu, mwana wa Hamori, Mhivi, mkuu wa nchi, akamwona akamtwaa, akalala naye, akambikiri.
3 Moyo wake ukaambatana na Dina binti Yakobo, akampenda huyu msichana, akasema na huyu msichana kwa maneno mazuri.
4 Shekemu akamwambia Hamori, babaye, akasema, Unipatie msichana huyu awe mke wangu.
5 Basi Yakobo akasikia ya kwamba amembikiri Dina, binti yake. Na wanawe walikuwako pamoja na wanyama wake nyikani. Yakobo akanyamaza, hata walipokuja.
6 Akatoka Hamori, babaye Shekemu, kumwendea Yakobo, aseme naye.
7 Wanawe Yakobo waliposikia hayo, wakaja kutoka nyikani; nao wakasikitika sana, wakakasirika mno, kwa sababu amefanya upumbavu katika Israeli kwa kulala na binti Yakobo, neno lisilojuzu kutendeka.