3 Ikawa hatimaye Kaini akaleta mazao ya ardhi, sadaka kwa BWANA.
4 Habili naye akaleta wazao wa kwanza wa wanyama wake na sehemu zilizonona za wanyama. BWANA akamtakabali Habili na sadaka yake;
5 bali Kaini hakumtakabali, wala sadaka yake. Kaini akaghadhibika sana, uso wake ukakunjamana.
6 BWANA akamwambia Kaini, Kwa nini una ghadhabu? Na kwa nini uso wako umekunjamana?
7 Kama ukitenda vyema, hutapata kibali? Usipotenda vyema dhambi iko, inakuotea mlangoni, nayo inakutamani wewe, walakini yapasa uishinde.
8 Kaini akamwambia Habili nduguye, [Twende uwandani]. Ikawa walipokuwapo uwandani, Kaini akamwinukia Habili nduguye, akamwua.
9 BWANA akamwambia Kaini, Yuko wapi Habili ndugu yako? Akasema, Sijui, mimi ni mlinzi wa ndugu yangu?