5 Maji yakapunguka-punguka hata mwezi wa kumi; mwezi huo wa kumi, siku ya kwanza ya mwezi, vilele vya milima vikaonekana.
6 Ikawa baada ya siku arobaini, Nuhu akalifungua dirisha la safina, alilolifanya;
7 akatoa kunguru, naye akatoka akaenda huko na huko, hata maji yakakauka juu ya nchi.
8 Kisha akatoa njiwa, aone kwamba maji yamepunguka usoni pa nchi;
9 bali yule njiwa hakuona mahali pa kutua kwa wayo wa mguu wake, akamrudia Nuhu safinani, maana maji yalikuwa juu ya uso wa nchi yote; naye akanyosha mkono, akamtwaa, akamwingiza mle safinani.
10 Akangoja na siku saba tena; kisha akamtoa yule njiwa katika safina mara ya pili,
11 njiwa akamjia jioni, na tazama, alikuwa na jani bichi la mzeituni kinywani mwake, ambalo amelitunda, basi Nuhu akajua ya kwamba maji yamepunguka juu ya nchi.