15 Kisha ikawa, adui zetu waliposikia ya kuwa tumekwisha kupata habari, na ya kuwa Mungu amelibatilisha shauri lao, ndipo sisi sote tukarudi ukutani, kila mtu kwa kazi yake.
16 Ikawa tokea wakati huo, nusu ya watumishi wangu walitumika katika kazi hiyo, na nusu yao wakaishika mikuki, na ngao, na pinde, na darii; na maakida walikuwa nyuma ya nyumba yote ya Yuda.
17 Watu wale walioujenga ukuta, na wale waliochukua mizigo, walijitweka wenyewe, kila mtu alifanya kazi kwa mkono mmoja, na kwa mkono wake wa pili alishika silaha yake;
18 nao wajenzi, kila mtu alikuwa na upanga wake, umefungwa ubavuni mwake, ndivyo alivyojenga. Na yeye aliyepiga baragumu alikuwa karibu na mimi.
19 Nikawaambia wakuu, na mashehe na watu wengine; Kazi hii ni nyingi, tena kubwa, nasi tumetawanyika juu ya ukuta, kila mtu mbali na mwenzake;
20 basi mahali po pote mtakaposikia sauti ya baragumu, enendeni huko, mkatujie; Mungu wetu atatupigania.
21 Hivyo tukajitia katika kazi hiyo; na nusu yao waliishika mikuki, tangu alfajiri hata nyota zikatokea.