24 Basi wale watoto wakaingia wakaimiliki nchi, nawe ukawatiisha wenyeji wa nchi mbele yao, ndio Wakanaani, ukawatia mikononi mwao, pamoja na wafalme wao, na watu wa nchi, wawatende kama wapendavyo.
25 Wakaitwaa miji yenye boma, na nchi yenye neema, wakazitamalaki nyumba zilizojaa vitu vyema, birika zilizochimbwa, mizabibu, na mizeituni, na miti mingi yenye matunda; hivyo wakala, wakashiba, wakanenepa, wakajifurahisha katika wema wako mwingi.
26 Walakini hawakukutii, wakakuasi, wakaitupa sheria yako nyuma yao, wakawaua manabii wako walioshuhudu juu yao wapate kuwarejeza kwako; wakatenda machukizo makuu.
27 Kwa sababu hiyo ukawatia katika mikono ya adui zao, waliowasumbua; na wakati wa shida yao, walipokulilia, uliwasikia kutoka mbinguni; na kwa wingi wa rehema zako ukawapa waokozi waliowaokoa katika mikono ya adui zao.
28 Lakini walipokuwa wamekwisha kustarehe, walitenda mabaya tena mbele zako; kwa hiyo ukawaacha katika mikono ya adui zao, nao wakawatawala; hata hivyo waliporejea na kukulilia, uliwasikia toka mbinguni; ukawaokoa mara nyingi kwa rehema zako;
29 ukawashuhudia ili uwarudishe tena katika sheria yako; lakini walitakabari, wasizisikilize amri zako, bali wakazihalifu hukumu zako, (ambazo mtu akizitenda ataishi katika hizo), nao wakayaondoa mabega yao, wakafanya shingo zao kuwa ngumu, wasitake kusikiliza.
30 Lakini miaka mingi ukachukuliana nao, nawe ukawashuhudia kwa roho yako kwa vinywa vya manabii wako; wao wasitake kusikiliza; kwa hiyo ukawatia katika mikono ya watu wa nchi.