8 Kisha Naomi akawaambia wakweze wawili, Nendeni sasa mkarejee kila mmoja nyumbani kwa mamaye; BWANA na awatendee mema ninyi, kama ninyi mlivyowatendea mema hao waliofariki na mimi pia.
9 BWANA na awajalie kuona raha kila mmoja nyumbani kwa mumewe. Kisha akawabusu; nao wakapaza sauti zao wakalia.
10 Wakamwambia, La, sivyo; lakini tutarudi pamoja nawe kwa watu wako.
11 Naye Naomi akasema, Enyi wanangu, mrejee; kwani kufuatana na mimi? Je! Mimi ninao watoto wa kiume tena tumboni mwangu, hata wawe waume zenu?
12 Enyi wanangu, mrejee; nendeni zenu; kwa kuwa mimi ni mzee, siwezi kupata mume tena. Kama ningesema, Natumaini; kama ningepata mume hata usiku huu, na kuzaa watoto wa kiume;
13 je! Mngesubiri hata watakapokuwa watu wazima? Mngejizuia msiwe na waume? La, sivyo, wanangu; maana ni vigumu kwangu kuliko kwenu, kwa sababu mkono wa BWANA umetoka juu yangu.
14 Nao wakapaza sauti zao, wakalia tena, na Orpa akambusu mkwewe, lakini Ruthu akaambatana naye.