4 Nami nitaunyosha mkono wangu juu ya Yuda, na juu ya watu wote wakaao Yerusalemu; nami nitayakatilia mbali mabaki ya Baali, yasionekane mahali hapa, na hilo jina la Wakemari pamoja na makuhani;
5 na wale walisujudiao jeshi la mbinguni juu ya dari za nyumba; na hao waabuduo, waapao kwa BWANA na kuapa pia kwa Malkamu;
6 na hao waliorudi nyuma, na kuacha kumfuata BWANA; na hao wasiomtafuta BWANA, wala kumwulizia.
7 Nyamaza kimya mbele za Bwana MUNGU;Kwa maana siku ya BWANA i karibu;Kwa kuwa BWANA ameweka tayari dhabihu,Amewatakasa wageni wake.
8 Na itakuwa, katika siku ile ya dhabihu ya BWANA, nitawaadhibu wakuu, na wana wa mfalme, na watu wote waliovaa mavazi ya kigeni.
9 Na katika siku ile nitawaadhibu hao wote warukao juu ya kizingiti, waijazao nyumba ya bwana wao udhalimu na udanganyifu.
10 Na katika siku ile, asema BWANA kutakuwako sauti ya kilio kutoka lango la samaki, na mlio mkuu katika mtaa wa pili, na mshindo mkuu kutoka milimani.