1 Jikusanyeni, naam, jikusanyeni, Ee taifa lisilo na haya;
2 kabla haijazaa hiyo amri, kabla haijapita siku ile kama makapi, kabla haijawajilia hasira kali ya BWANA, kabla haijawajilia siku ya hasira ya BWANA.
3 Mtafuteni BWANA, enyi nyote mlio wanyenyekevu wa dunia, ninyi mliozitenda hukumu zake; itafuteni haki, utafuteni unyenyekevu; huenda mtafichwa katika siku ya hasira ya BWANA.
4 Kwa kuwa Gaza utaachwa, na Ashkeloni utakuwa ukiwa; wataufukuzia mbali Ashdodi wakati wa adhuhuri, na Ekroni utang’olewa. Amo 1:6-8; Zek 9:5-7
5 Ole wao wakaao karibu na pwani ya bahari, taifa la Wakerethi! Neno la BWANA li juu yenu, Ee Kanaani, nchi ya Wafilisti; mimi nitakuangamiza, asibaki mtu akaaye kwako.
6 Na hiyo nchi ya pwani itakuwa malisho, yenye vibanda vya wachungaji, na mazizi ya makundi ya kondoo.
7 Na hiyo nchi ya pwani itakuwa nchi ya watu wa nyumba ya Yuda waliosalia; watalisha makundi yao huko; watalala katika nyumba za Ashkeloni wakati wa jioni; kwa maana BWANA, Mungu wao, atawajilia na kuwarudisha wafungwa wao.