8 ikiwa taifa lile nililolitaja litageuka, na kuacha maovu yake nitaghairi, nisitende mabaya yale niliyoazimia kuwatenda.
9 Na wakati wo wote nitakapotoa habari za taifa, na habari za ufalme, kuujenga na kuupanda,
10 ikiwa watatenda maovu mbele za macho yangu, wasiitii sauti yangu, basi nitaghairi, nisitende mema yale niliyoazimia kuwatendea.
11 Haya! Basi, ukawaambie watu wa Yuda, na wenyeji wa Yerusalemu, ukisema, BWANA asema hivi, Tazama, ninafinyanga mabaya juu yenu, na kuwaza mawazo juu yenu; rudini sasa, kila mmoja na aiache njia yake mbaya; zitengenezeni njia zenu, na matendo yenu.
12 Lakini wao wasema, Hapana tumaini lo lote; maana sisi tutafuata mawazo yetu wenyewe, nasi tutatenda kila mmoja wetu kwa kuufuata ushupavu wa moyo wake mbaya.
13 Basi, kwa ajili ya hayo, BWANA asema hivi, Ulizeni sasa katika mataifa, ni nani aliyesikia habari za mambo kama hayo; bikira wa Israeli ametenda tendo lichukizalo sana.
14 Je! Theluji ya Lebanoni itakoma katika jabali la kondeni? Au je! Maji ya baridi yashukayo toka mbali yatakauka?