1 Wakati huo, asema BWANA, nitakuwa Mungu wa jamaa zote za Israeli, nao watakuwa watu wangu.
2 BWANA asema hivi, Watu wale walioachwa na upanga walipata neema jangwani; yaani, Israeli, hapo nilipokwenda kumstarehesha.
3 BWANA alinitokea zamani, akisema, Naam nimekupenda kwa upendo wa milele, ndiyo maana nimekuvuta kwa fadhili zangu.
4 Mara ya pili nitakujenga, nawe utajengwa, Ee bikira wa Israeli mara ya pili utapambwa kwa matari yako, nawe utatokea katika michezo yao wanaofurahi.
5 Mara ya pili utapanda mizabibu juu ya milima ya Samaria; wapanzi watapanda, nao watayafurahia matunda yake.
6 Maana kutakuwa siku moja, ambayo walinzi watalia juu ya vilima vya Efraimu, Inukeni, tukaende Sayuni, kwa BWANA, Mungu wetu.
7 Maana BWANA asema hivi, Mwimbieni Yakobo kwa furaha, mkampigie kelele mkuu wa mataifa, tangazeni, sifuni, mkaseme, Ee BWANA, uwaokoe watu wako, mabaki ya Israeli.
8 Tazama, nitawaleta toka nchi ya kaskazini, na kuwakusanya katika miisho ya dunia, na pamoja nao watakuja walio vipofu, na hao wachechemeao, mwanamke mwenye mimba, na yeye pia aliye na utungu wa kuzaa; watarudi huko, jeshi kubwa.
9 Watakuja kwa kulia, na kwa maombi nitawaongoza; nitawaendesha penye mito ya maji, katika njia iliyonyoka; katika njia hiyo hawatajikwaa; maana mimi ni baba wa Israeli, na Efraimu ni mzaliwa wa kwanza wangu.
10 Lisikieni neno la BWANA, enyi mataifa, litangazeni visiwani mbali; mkaseme, Aliyemtawanya Israeli atamkusanya, na kumlinda, kama mchungaji alindavyo kundi lake.
11 Kwa maana BWANA amemweka huru Yakobo, amemkomboa mkononi mwake aliyekuwa hodari kuliko yeye.
12 Nao watakuja, na kuimba katika mlima Sayuni, wataukimbilia wema wa BWANA, nafaka, na divai, na mafuta, na wachanga wa kondoo na wa ng’ombe; na roho zao zitakuwa kama bustani iliyotiwa maji; wala hawatahuzunika tena kabisa.
13 Ndipo bikira atafurahi katika kucheza, na vijana na wazee pamoja; maana nitageuza masikitiko yao kuwa furaha, nami nitawafariji, na kuwafurahisha waache huzuni zao.
14 Nami nitaishibisha roho ya makuhani kwa unono, na watu wangu watashiba kwa wema wangu, asema BWANA
15 BWANA asema hivi,Sauti imesikiwa Rama,kilio, na maombolezo mengi,Raheli akiwalilia watoto wake;asikubali kufarijiwa kwa watoto wake, kwa kuwa hawako,
16 BWANA asema hivi,Zuia sauti yako, usilie,na macho yako yasitoke machozi;Maana kazi yako itapata thawabu,nao watakuja tena toka nchi ya adui;Ndivyo asemavyo BWANA.
17 Tena liko tumaini kwa siku zako za mwisho, asema BWANA; na watoto wako watarejea hata mpaka wao wenyewe.
18 Hakika nimemsikia Efraimu, akijililia hivi, Umeniadhibu, nami nikaadhibika, kama ndama asiyeizoelea nira; unigeuze, nami nitageuzwa; kwa maana wewe u BWANA, Mungu wangu.
19 Hakika baada ya kugeuzwa kwangu, nalitubu; na baada ya kufundishwa kwangu, nalijipiga pajani; nalitahayarika, naam, nalifadhaika, kwa sababu naliichukua aibu ya ujana wangu.
20 Je! Efraimu siye mwanangu mpendwa? Je! Siye mtoto apendezaye? Maana kila nisemapo neno juu yake, ningali nikimkumbuka sana; kwa sababu hiyo moyo wangu unataabika kwa ajili yake; bila shaka nitamrehemu, asema BWANA.
21 Jiwekee alama za njia; jifanyie miti ya kukuongoza; uuelekeze moyo wako kwenye njia kuu, njia ile ile uliyoiendea; rudi tena, Ee bikira wa Israeli, irudie hii miji yako.
22 Hata lini utatanga-tanga, Ee binti mwenye kuasi? Kwa maana BWANA ameumba jambo jipya duniani; mwanamke atamlinda mwanamume.
23 BWANA wa majeshi, Mungu wa Israeli, asema hivi, Watatumia tena neno hili katika nchi ya Yuda, na katika miji yake, nitakapowarudisha mateka yao; BWANA na akubariki, Ee kao la haki, Ee mlima wa utakatifu.
24 Na Yuda, na miji yake yote, watakaa humo pamoja; wakulima, nao waendao huko na huko pamoja na makundi yao.
25 Kwa maana nimeishibisha roho yenye uchovu, nami nimeiridhisha kila roho yenye huzuni.
26 Basi, nikaamka, nikaangalia; na usingizi wangu ulikuwa mtamu kwangu.
27 Tazama, siku zinakuja, asema BWANA, nitakapoipanda nyumba ya Israeli, na nyumba ya Yuda, mbegu ya mwanadamu na mbegu ya mnyama.
28 Tena itakuwa, kwa kadiri nilivyowaangalia, ili kung’oa, na kubomoa, na kuangusha, na kuangamiza, na kutesa; kwa kadiri iyo hiyo nitawaangalia, ili kujenga, na kupanda, asema BWANA.
29 Siku zile, hawatasema tena, Baba za watu wamekula zabibu kali, na meno ya watoto wao yametiwa ganzi.
30 Bali kila mtu atakufa kwa sababu ya uovu wake mwenyewe; kila mtu alaye zabibu kali, meno yake yatatiwa ganzi.
31 Angalia, siku zinakuja, asema BWANA, nitakapofanya agano jipya na nyumba ya Israeli, na nyumba ya Yuda.
32 Si kwa mfano wa agano lile nililolifanya na baba zao, katika siku ile nilipowashika mkono, ili kuwatoa katika nchi ya Misri; ambalo agano langu hilo walilivunja, ingawa nalikuwa mume kwao, asema BWANA.
33 Bali agano hili ndilo nitakalofanya na nyumba ya Israeli, baada ya siku zile, asema BWANA; Nitatia sheria yangu ndani yao, na katika mioyo yao nitaiandika; nami nitakuwa Mungu wao, nao watakuwa watu wangu.
34 Wala hawatamfundisha kila mtu jirani yake, na kila mtu ndugu yake, wakisema, Mjue BWANA; kwa maana watanijua wote, tangu mtu aliye mdogo miongoni mwao hata aliye mkubwa miongoni mwao, asema BWANA; maana nitausamehe uovu wao, wala dhambi yao sitaikumbuka tena.
35 BWANA asema hivi, awapaye watu jua, ili kuwa nuru wakati wa mchana, na amri za mwezi na nyota, ili kuwa nuru wakati wa usiku, aichafuaye bahari, hata mawimbi yake yakavuma; BWANA wa majeshi, ndilo jina lake;
36 Amri hizi zikiondoka, zisiwe mbele zangu, asema BWANA, ndipo wazao wa Israeli nao wataacha kuwa taifa mbele zangu milele.
37 BWANA asema hivi, Kama mbingu zikiweza kupimwa, na misingi ya dunia ikiweza kugunduliwa huko chini, ndipo wazao wa Israeli pia nitawatupilia mbali, kwa ajili ya hayo yote waliyoyatenda, asema BWANA.
38 Tazama, siku zinakuja, asema BWANA, mji huu utakapojengwa kwa ajili ya BWANA, toka buruji ya Hananeli hata lango la pembeni.
39 Na kamba ya kupimia itaendelea moja kwa moja hata mlima Garebu, tena itazunguka na kufika Goa.
40 Na bonde lote la mizoga, na majivu, na mashamba yote mpaka kijito Kidroni, mpaka pembe ya lango la farasi, upande wa mashariki, patakuwa patakatifu kwa BWANA; hapatang’olewa, wala hapatabomolewa, hata milele.