1 Neno hili ndilo ambalo Yeremia, nabii, alimwambia Baruku, mwana wa Neria, alipoyaandika maneno haya katika kitabu kwa kinywa cha Yeremia, mwaka wa nne wa Yehoyakimu, mwana wa Yosia, mfalme wa Yuda, kusema,
2 BWANA, Mungu wa Israeli, akuambia wewe Ee Baruku;
3 Ulisema, Ole wangu! Kwa maana BWANA ameongeza huzuni pamoja na maumivu yangu. Nimechoka kwa ajili ya kuugua kwangu, wala sioni raha.
4 Basi, mwambie hivi, BWANA asema hivi, Tazama, niliyoyajenga nitayabomoa, na niliyoyapanda nitayang’oa; na haya yatakuwa katika nchi yote.
5 Je! Unajitafutia mambo makuu? Usiyatafute; kwa maana tazama, nitaleta mabaya juu ya wote wenye mwili, asema BWANA; lakini roho yako nitakupa iwe nyara, katika mahali pote utakapokwenda.