14 Katika manabii wa Yerusalemu nimeona neno linalochukiza sana; hufanya zinaa; huenenda katika maneno ya uongo, hutia nguvu mikono ya watendao maovu, hata ikawa hapana mtu arejeaye na kuuacha uovu wake; wote pia wamekuwa kama Sodoma kwangu, na wenyeji wake kama Gomora.
15 Basi BWANA wa majeshi asema hivi, katika habari ya manabii, Tazama, nitawalisha pakanga, nitawanywesha maji ya uchungu; kwa kuwa kutoka kwa manabii hao wa Yerusalemu kukufuru kumeingia katika nchi yote.
16 BWANA wa majeshi asema hivi, Msisikilize maneno ya manabii wakiwatabiria; huwafundisha ubatili; hunena maono ya mioyo yao wenyewe; hayakutoka katika kinywa cha BWANA.
17 Daima huwaambia wao wanaonidharau, BWANA amesema, Mtakuwa na amani; nao humwambia kila mtu aendaye kwa ukaidi wa moyo wake, Hamtapatwa na ubaya wo wote.
18 Maana, ni nani aliyesimama katika baraza la BWANA, hata akalifahamu neno lake na kulisikia? Ni nani aliyelitia moyoni neno langu, na kulisikia?
19 Tazama, tufani ya BWANA, yaani, ghadhabu yake, imetokea; ni dhoruba ya kisulisuli; itapasuka, na kuwaangukia waovu vichwani.
20 Hasira ya BWANA haitarudi, hata atakapokwisha kuyatimiza makusudi ya moyo wake; katika siku za mwisho mtalifahamu neno hili kabisa.