16 BWANA wa majeshi asema hivi, Msisikilize maneno ya manabii wakiwatabiria; huwafundisha ubatili; hunena maono ya mioyo yao wenyewe; hayakutoka katika kinywa cha BWANA.
17 Daima huwaambia wao wanaonidharau, BWANA amesema, Mtakuwa na amani; nao humwambia kila mtu aendaye kwa ukaidi wa moyo wake, Hamtapatwa na ubaya wo wote.
18 Maana, ni nani aliyesimama katika baraza la BWANA, hata akalifahamu neno lake na kulisikia? Ni nani aliyelitia moyoni neno langu, na kulisikia?
19 Tazama, tufani ya BWANA, yaani, ghadhabu yake, imetokea; ni dhoruba ya kisulisuli; itapasuka, na kuwaangukia waovu vichwani.
20 Hasira ya BWANA haitarudi, hata atakapokwisha kuyatimiza makusudi ya moyo wake; katika siku za mwisho mtalifahamu neno hili kabisa.
21 Mimi sikuwatuma manabii hao, lakini walikwenda mbio; sikusema nao, lakini walitabiri.
22 Lakini kama wangalisimama katika baraza yangu, ndipo wangaliwasikizisha watu wangu maneno yangu, na kuwageuza waziache njia zao mbaya, na uovu wa matendo yao.