8 Na itakuwa, taifa lile na mfalme yule asiyetaka kumtumikia Nebukadreza, huyo mfalme wa Babeli, na kutia shingo zao katika nira ya mfalme wa Babeli, mimi nitaliadhibu taifa lile kwa upanga, na kwa njaa, na kwa tauni, asema BWANA, hata nitakapokuwa nimewaangamiza kwa mkono wake.
9 Lakini, katika habari zenu, msisikilize manabii wenu, wala wabashiri wenu, wala ndoto zenu, wala watambuzi wenu, wala waganga wenu, wanaowaambia, ya kwamba, Hamtamtumikia mfalme wa Babeli;
10 maana wanawatabiria uongo, ili kuwatoa ninyi mbali na nchi yenu; niwafukuze mkaangamie.
11 Bali taifa lile watakaotia shingo zao katika nira ya mfalme wa Babeli, na kumtumikia, taifa hilo nitawaacha wakae katika nchi yao wenyewe, asema BWANA; nao watailima, na kukaa ndani yake.
12 Nikamwambia Sedekia, mfalme wa Yuda, kwa mfano wa maneno hayo yote, nikisema, Tieni shingo zenu katika nira ya mfalme wa Babeli, mkamtumikie yeye na watu wake, mpate kuishi.
13 Mbona mnataka kufa, wewe na watu wako, kwa upanga, na kwa njaa, na kwa tauni, kama BWANA alivyosema katika habari ya taifa lile, lisilotaka kumtumikia mfalme wa Babeli?
14 Wala msisikilize maneno ya manabii wawaambiao ninyi, ya kwamba, Hamtamtumikia mfalme wa Babeli; maana wanawatabiria uongo.