1 Neno hili ndilo lililomjia Yeremia, kutoka kwa BWANA, baada ya wakati ule Nebuzaradani, amiri wa askari walinzi, alipomwacha aende zake toka Rama, baada ya kumchukua hali ya kufungwa minyororo, pamoja na wafungwa wote wa Yerusalemu na Yuda, waliochukuliwa hali ya kufungwa mpaka Babeli.
2 Naye amiri wa askari walinzi akamtwaa Yeremia, akamwambia, BWANA, Mungu wako, alitamka mabaya haya juu ya mahali hapa;
3 naye BWANA ameyaleta, na kufanya kama alivyosema; kwa sababu mmemwasi BWANA, wala hamkuitii sauti yake; ndiyo maana neno hili limewajia ninyi.
4 Na sasa, tazama, nakufungulia leo minyororo hii iliyo mikononi mwako. Kama ukiona ni vema kwenda Babeli pamoja nami, haya! Njoo, nami nitakutunza sana; lakini kama ukiona ni vibaya kwenda Babeli pamoja nami, basi, acha; tazama, nchi yote i mbele yako; palipo pema machoni pako na pa kukufaa, enenda huko.