17 Nao watakula mavuno yako, na mkate wako, ambao iliwapasa wana wako na binti zako kuula; watakula makundi yako ya kondoo na ya ng’ombe; watakula mizabibu yako na mitini yako; wataiharibu miji yako yenye boma, uliyokuwa ukiitumainia, naam, wataiharibu kwa upanga.
18 Lakini hata katika siku zile, asema BWANA, sitawakomesha ninyi kabisa.
19 Tena itakuwa mtakapouliza, BWANA ametutenda mambo hayo yote kwa sababu gani? Ndipo utakapowaambia, Vile vile kama ninyi mlivyoniacha mimi, na kuwatumikia miungu mingine katika nchi yenu wenyewe, ndivyo mtakavyowatumikia wageni katika nchi isiyo yenu.
20 Tangazeni neno hili katika nyumba ya Yakobo, litangazeni katika Yuda, kusema,
21 Sikilizeni neno hili, enyi watu wajinga msio na ufahamu; mlio na macho ila hamwoni; mlio na masikio ila hamsikii.
22 Je! Hamniogopi mimi? Asema BWANA; hamtatetemeka mbele za uso wangu; mimi niliyeweka mchanga kuwa mpaka wa bahari, kwa amri ya daima, isiweze kuupita? Mawimbi yake yajapoumuka-umuka, hayawezi kushinda nguvu; yajapovuma sana, hayawezi kuupita.
23 Lakini watu hawa wana moyo wa kuasi na ukaidi; wameasi, wamekwenda zao.