11 Kwa sababu mnafurahi, kwa sababu mnashangilia, enyi mnaouteka urithi wangu, kwa sababu mmewanda kama mtamba akanyagaye nafaka, nanyi mnalia kama farasi wenye nguvu;
12 mama yenu atatahayarika sana; yeye aliyewazaa atafadhaika; tazama, atakuwa taifa lililo nyuma katika mataifa yote, atakuwa jangwa, nchi ya ukame, na nyika.
13 Kwa sababu ya ghadhabu ya BWANA haitakaliwa na mtu, bali itakuwa ukiwa mtupu; kila mtu apitaye karibu na Babeli atashangaa, atazomea kwa sababu ya mapigo yake yote.
14 Jipangeni juu ya Babeli pande zote,Ninyi nyote mpindao upinde;Mpigeni, msiuzuie hata mshale mmoja;Kwa maana amemtenda BWANA dhambi.
15 Mpigieni kelele pande zote; amejitoa;Maboma yake yameanguka, kuta zake zimebomolewa;Kwa maana ni kisasi cha BWANA; mlipizeni kisasi;Kama yeye alivyotenda, mtendeni yeye.
16 Mpanzi mkatilie mbali na Babeli,Naye ashikaye mundu wakati wa mavuno;Kwa sababu ya kuuogopa upanga uoneao,Watageuka kila mtu kwa watu wake,Nao wataikimbilia kila mmoja nchi yake.
17 Israeli ni kondoo aliyetawanywa; simba wamemfukuzia mbali; kwanza mfalme wa Ashuru amemla, na mwisho Nebukadreza huyu, mfalme wa Babeli, amemvunja mifupa yake.