9 Kwa maana juu ya Babeli nitaamsha na kuleta kusanyiko la mataifa makubwa, toka nchi ya kaskazini; nao watajipanga juu yake; kutoka huko atatwaliwa; mishale yao itakuwa kama ya mtu shujaa aliye stadi; hapana hata mmoja utakaorudi bure.
10 Nao Ukaldayo utakuwa mateka; wote wautekao watashiba, asema BWANA.
11 Kwa sababu mnafurahi, kwa sababu mnashangilia, enyi mnaouteka urithi wangu, kwa sababu mmewanda kama mtamba akanyagaye nafaka, nanyi mnalia kama farasi wenye nguvu;
12 mama yenu atatahayarika sana; yeye aliyewazaa atafadhaika; tazama, atakuwa taifa lililo nyuma katika mataifa yote, atakuwa jangwa, nchi ya ukame, na nyika.
13 Kwa sababu ya ghadhabu ya BWANA haitakaliwa na mtu, bali itakuwa ukiwa mtupu; kila mtu apitaye karibu na Babeli atashangaa, atazomea kwa sababu ya mapigo yake yote.
14 Jipangeni juu ya Babeli pande zote,Ninyi nyote mpindao upinde;Mpigeni, msiuzuie hata mshale mmoja;Kwa maana amemtenda BWANA dhambi.
15 Mpigieni kelele pande zote; amejitoa;Maboma yake yameanguka, kuta zake zimebomolewa;Kwa maana ni kisasi cha BWANA; mlipizeni kisasi;Kama yeye alivyotenda, mtendeni yeye.