1 Kisha mkutano mzima wa wana wa Israeli walikutana pamoja hapo Shilo, wakasimamisha hema ya kukutania kuko; nayo nchi ilikuwa imeshindwa mbele zao.
2 Zilisalia katika wana wa Israeli kabila saba ambazo hazijagawanyiwa bado urithi wao.
3 Yoshua akawauliza wana wa Israeli, akasema, Je! Hata lini mtakuwa walegevu katika kuingia kwenu na kuimiliki hiyo nchi, ambayo yeye BWANA, Mungu wa baba zenu, amewapa?
4 Haya, jichagulieni watu watatu kwa ajili ya kila kabila; nami nitawatuma, nao watainuka waende kati ya hiyo nchi, na kuiandika kama urithi wao ulivyo; kisha watanijilia mimi.
5 Watu hao wataigawanya nchi iwe mafungu saba; Yuda atakaa katika mpaka wake huko upande wa kusini, na nyumba ya Yusufu watakaa katika mpaka wao upande wa kaskazini.
6 Nanyi mtaiandika nchi iwe mafungu saba, kisha hayo maandiko yake mtaniletea mimi hapa; nami nitawapigia kura hapa mbele ya BWANA, Mungu wetu.
7 Kwa maana Walawi hawana fungu kati yenu; Kwa kuwa huo ukuhani wa BWANA ndio urithi wao; tena Gadi, na Reubeni, na hiyo nusu ya kabila ya Manase, wamekwisha pata urithi wao ng’ambo ya pili ya Yordani upande wa mashariki, ambao walipewa na Musa, mtumishi wa BWANA.