12 Basi sasa, nawasihi, niapieni kwa BWANA, kwa kuwa nimewatendea ihisani, ya kwamba ninyi nanyi mtaitendea ihisani nyumba ya baba yangu; tena nipeni alama ya uaminifu;
13 ya kwamba mtawaponya hai baba yangu na mama yangu, na ndugu zangu wanaume na wanawake, na vitu vyote walivyo navyo, na kutuokoa roho zetu na kufa.
14 Wale wanaume wakamwambia, Uhai wetu badala ya uhai wenu, ikiwa hamwitangazi habari ya shughuli yetu hii; kisha itakuwa, wakati BWANA atakapotupa nchi hii, tutakutendea kwa ihisani na uaminifu.
15 Ndipo akawashusha kwa kamba dirishani, maana nyumba yake ilikuwa katika ukuta wa mji; naye alikaa ukutani.
16 Akawaambia, Enendeni zenu mlimani, wale wanaowafuatia wasije wakawapata; mkajifiche huko siku tatu hata wao wanaowafuatia watakaporudi; kisha enendeni zenu.
17 Wale wanaume wakamwambia, Sisi tunataka tusiwe na hatia kwa ajili ya kiapo hiki ulichotuapisha.
18 Angalia, tutakapoingia katika nchi hii, funga kamba hii nyekundu katika dirisha hili ulilotutelemshia; nawe uwakusanye kwako nyumbani mwako, baba yako, na mama yako, na ndugu zako, na watu wote wa nyumba ya baba yako.