1 Katika siku hiyo watu wa nyumba ya Daudi, na wenyeji wa Yerusalemu, watafunguliwa chemchemi kwa dhambi na kwa unajisi.
2 Kisha itakuwa katika siku hiyo, asema BWANA wa majeshi, nitakatilia mbali majina ya sanamu katika nchi, yasikumbukwe tena; pia nitawafukuza manabii, na roho ya uchafu, watoke katika nchi.
3 Tena itakuwa ya kwamba, mtu awaye yote atakapotoa unabii, basi baba yake na mama yake waliomzaa watamwambia, Hutaishi; kwa maana unanena maneno ya uongo kwa jina la BWANA; na baba yake na mama yake waliomzaa watamtumbua atoapo unabii.
4 Tena itakuwa siku hiyo, ya kwamba manabii, kila mmoja wao, atayaonea haya maono yake atoapo unabii; wala hawatavaa joho ya nywele ili kudanganya watu;
5 bali atasema, Mimi si nabii kamwe; mimi ni mkulima wa nchi; kwa maana nalifanywa mtumwa tokea ujana wangu.