1 Ikawa katika mwaka wa nne wa mfalme Dario, neno la BWANA lilimjia Zekaria, siku ya nne ya mwezi wa kenda, yaani, Kisleu.
2 Basi watu wa Betheli walikuwa wamewatuma Shareza na Regem-meleki, na watu wao, ili kuomba fadhili za BWANA,
3 na kusema na makuhani wa nyumba ya BWANA wa majeshi, na hao manabii, ya kwamba, Je! Yanipasa kulia katika mwezi wa tano, na kujitenga na watu, kama nilivyofanya miaka hii mingi iliyopita?
4 Ndipo neno la BWANA wa majeshi likanijia, kusema,
5 Waambie watu wote wa nchi, na hao makuhani, ukisema, Hapo mlipofunga na kuomboleza katika mwezi wa tano na mwezi wa saba, katika miaka hiyo sabini, je! Mlinifungia mimi kwa lo lote; mlinifungia mimi?
6 Na wakati mlapo chakula na kunywa, je! Hamli kwa ajili ya nafsi zenu, na kunywa kwa ajili ya nafsi zenu?