2 BWANA wa majeshi asema hivi, Mimi nina wivu kwa ajili ya Sayuni, wivu mkuu, nami nina wivu kwa ajili yake kwa ghadhabu kuu.
3 BWANA asema hivi, Mimi nimerudi Sayuni, nami nitakaa katikati ya Yerusalemu; na Yerusalemu utaitwa, Mji wa kweli; na Mlima wa BWANA wa majeshi utaitwa, Mlima mtakatifu.
4 BWANA wa majeshi asema hivi, Wazee wanaume na wazee wanawake watakaa tena katika njia za Yerusalemu, kila mtu ana mkongojo wake mkononi, kwa kuwa ni mzee sana.
5 Na hizo njia za mji zitajaa wavulana, na wasichana, wakicheza katika njia zake.
6 BWANA wa majeshi asema hivi, Ingawa hili ni neno lililo gumu mbele ya macho ya mabaki ya watu hawa katika siku hizo, je! Liwe neno gumu mbele ya macho yangu? Asema BWANA wa majeshi.
7 BWANA wa majeshi asema hivi, Tazama, nitawaokoa watu wangu toka nchi ya mashariki, na toka nchi ya magharibi;
8 nami nitawaleta, nao watakaa katikati ya Yerusalemu; nao watakuwa watu wangu, nami nitakuwa Mungu wao, katika kweli na katika haki.