4 BWANA wa majeshi asema hivi, Wazee wanaume na wazee wanawake watakaa tena katika njia za Yerusalemu, kila mtu ana mkongojo wake mkononi, kwa kuwa ni mzee sana.
5 Na hizo njia za mji zitajaa wavulana, na wasichana, wakicheza katika njia zake.
6 BWANA wa majeshi asema hivi, Ingawa hili ni neno lililo gumu mbele ya macho ya mabaki ya watu hawa katika siku hizo, je! Liwe neno gumu mbele ya macho yangu? Asema BWANA wa majeshi.
7 BWANA wa majeshi asema hivi, Tazama, nitawaokoa watu wangu toka nchi ya mashariki, na toka nchi ya magharibi;
8 nami nitawaleta, nao watakaa katikati ya Yerusalemu; nao watakuwa watu wangu, nami nitakuwa Mungu wao, katika kweli na katika haki.
9 BWANA wa majeshi asema hivi, Mikono yenu na iwe hodari, ninyi mnaosikia siku hizi maneno haya kwa vinywa vya manabii, waliokuwapo siku hiyo ulipowekwa msingi wa nyumba ya BWANA wa majeshi; yaani, hekalu hilo; ili lijengwe.
10 Maana kabla ya siku zile hapakuwa na ijara kwa mwanadamu, wala hapakuwa na ijara kwa mnyama; wala hapakuwa na amani kwake yeye aliyetoka, wala kwake yeye aliyeingia, kwa sababu ya adui; nami nalimwacha kila mtu kugombana na jirani yake.