1 Mimi Paulo, mfungwa kwa ajili ya Kristo Yesu, na ndugu Timotheo, ninakuandikia wewe Filemoni mpendwa, mfanyakazi mwenzetu,
2 na kanisa linalokutana nyumbani kwako, na wewe dada Afia, na askari mwenzetu Arkipo.
3 Tunawatakieni neema na amani kutoka kwa Mungu Baba yetu, na kwa Bwana Yesu Kristo.
4 Kila wakati ninaposali, nakukumbuka wewe Filemoni, na kumshukuru Mungu,
5 maana nasikia habari za imani yako kwa Bwana Yesu na upendo wako kwa watu wote wa Mungu.
6 Naomba ili imani hiyo unayoshiriki pamoja nasi ikuwezeshe kuwa na ujuzi mkamilifu zaidi wa baraka zote tunazopata katika kuungana kwetu na Kristo.
7 Ndugu, upendo wako umeniletea furaha kubwa na kunipa moyo sana! Nawe umeichangamsha mioyo ya watu wa Mungu.
8 Kwa sababu hiyo, ningeweza, kwa uhodari kabisa, nikiwa ndugu yako katika kuungana na Kristo, kukuamuru ufanye unachopaswa kufanya.
9 Lakini kwa sababu ya upendo, ni afadhali zaidi nikuombe. Nafanya hivi ingawa mimi ni Paulo, balozi wa Kristo Yesu, na sasa pia mfungwa kwa ajili yake.
10 Basi, ninalo ombi moja kwako kuhusu mwanangu Onesimo, ambaye ni mwanangu katika Kristo kwani nimekuwa baba yake nikiwa kifungoni.
11 Ni Onesimo yuleyule ambaye wakati mmoja alikuwa hakufai kitu, lakini sasa ananifaa mimi na wewe pia.
12 Sasa namrudisha kwako, naye ni kama moyo wangu mimi mwenyewe.
13 Ningependa akae nami hapa anisaidie badala yako wakati niwapo kifungoni kwa sababu ya Injili.
14 Lakini sitafanya chochote bila kibali chako. Sipendi kukulazimisha unisaidie, kwani wema wako unapaswa kutokana na hiari yako wewe mwenyewe na si kwa kulazimika.
15 Labda Onesimo aliondoka kwako kwa kitambo tu, kusudi uweze tena kuwa naye daima.
16 Na sasa yeye si mtumwa wa kawaida, ila ni bora zaidi ya mtumwa: Yeye ni ndugu yetu mpenzi. Ni wa maana sana kwangu mimi, na kwako atakuwa wa maana zaidi, kama mtumwa na kama ndugu katika Bwana.
17 Basi, ikiwa wanitambua mimi kuwa mwenzako, mpokee tena kama vile ungenipokea mimi mwenyewe.
18 Kama alikuwa amekukosea kitu, au alikuwa na deni lako, basi, unidai mimi.
19 Naandika jambo hili kwa mkono wangu mwenyewe: Mimi Paulo nitalipa! (Tena sina haja ya kusema kwamba wewe unalo deni kwangu la nafsi yako).
20 Naam, ndugu yangu, nifanyie jambo hilo kwa ajili ya jina la Bwana; burudisha moyo wangu kama ndugu katika Kristo.
21 Naandika nikitumaini kwamba utanikubalia ombi langu; tena najua kwamba utafanya hata zaidi ya haya ninayokuomba.
22 Pamoja na hayo, nitayarishie chumba kwani natumaini kwamba kwa sala zenu, Mungu atanijalia niwatembeleeni.
23 Epafra, mfungwa mwenzangu kwa ajili ya Kristo Yesu, anakusalimu.
24 Nao akina Marko, Aristarko, Dema na Luka, wafanyakazi wenzangu, wanakusalimu.
25 Nawatakieni nyinyi nyote neema ya Bwana Yesu Kristo.