13 Lakini malaika akamwambia, “Zakaria, usiogope, kwa maana sala yako imesikilizwa, na Elisabeti mkeo atakuzalia mtoto wa kiume, nawe utampa jina Yohane.
14 Utakuwa na furaha kubwa na watu wengi watashangilia kwa sababu ya kuzaliwa kwake.
15 Atakuwa mkubwa mbele ya Bwana. Hatakunywa divai wala kileo, atajazwa Roho Mtakatifu tangu tumboni mwa mama yake.
16 Atawaelekeza wengi wa watu wa Israeli kwa Bwana Mungu wao.
17 Atamtangulia Bwana akiongozwa na nguvu na roho kama ya Elia. Atawapatanisha kina baba na watoto wao; atawafanya wasiotii wawe na fikira za uadilifu, na hivyo amtayarishie Bwana watu wake.”
18 Zakaria akamwambia huyo malaika, “Ni kitu gani kitakachonihakikishia jambo hilo? Mimi ni mzee, hali kadhalika na mke wangu.”
19 Malaika akamjibu, “Mimi ni Gabrieli, nisimamaye mbele ya Mungu; nimetumwa niseme nawe, nikuletee hizi habari njema.