34 Akamwendea, akamtibu majeraha yake kwa kumtia mafuta na divai na kuyafunga; halafu akampandisha juu ya punda wake, akampeleka katika nyumba moja ya wageni akamwuguza.
35 Kesho yake akatoa fedha dinari mbili akampa yule mwenye nyumba, akamwambia, ‘Mwuguze mtu huyu; na chochote utakachotumia zaidi, nitakulipa nitakaporudi.’”
36 Kisha Yesu akauliza, “Kati ya hao watatu, ni yupi aliyeonesha kuwa jirani yake yule aliyevamiwa na majambazi?”
37 Yule mwalimu wa sheria akamjibu, “Ni yule aliyemwonea huruma.” Yesu akamwambia, “Nenda ukafanye vivyo hivyo.”
38 Walipokuwa safarini, waliingia katika kijiji kimoja na mwanamke mmoja aitwaye Martha, akamkaribisha nyumbani kwake.
39 Martha alikuwa na dada yake aitwaye Maria; huyu aliketi karibu na Yesu akisikiliza mafundisho yake.
40 Lakini Martha alikuwa anashughulika na mambo mengi. Basi, akamwendea Yesu, akamwambia, “Bwana, hivi hujali kwamba dada yangu ameniacha nishughulike peke yangu? Mwambie basi, anisaidie.”