32 “Msiogope, enyi kundi dogo! Maana Baba yenu amependa kuwapeni ufalme.
33 Uzeni mali yenu mkawape maskini hizo fedha. Jifanyieni mifuko isiyochakaa, na kujiwekea hazina mbinguni ambako haitapungua. Huko wezi hawakaribii, wala nondo hawaharibu.
34 Pale ilipo hazina yako, ndipo pia utakapokuwa moyo wako.
35 “Muwe tayari mmejifunga mkanda kiunoni, na taa zenu ziwe zinawaka;
36 muwe kama watumishi wanaomngojea bwana wao arudi kutoka harusini, ili wamfungulie mara atakapobisha.
37 Heri yao watumishi wale ambao bwana wao atakaporudi atawakuta wanakesha! Nawaambieni hakika, huyo bwana atajifunga mkanda kiunoni, atawaketisha mezani na kuwahudumia.
38 Hata kama atarudi usiku wa manane au alfajiri na kuwakuta wanakesha, heri yao watumishi hao!